AFYA

WANAWAKE LINDI KIKWAZO KUMALIZA UKATILI WA KIJINSIA

on

Na. Ahmad Mmow, Kilwa Kivinje.

Miongoni mwa sababu za kushamiri ukatili wa kijinsia mkoani Lindi ni huruma ya wanawake kwa waume zao kwa kushindwa kuwachukilia hatua za kisheria wanapofanyiwa vitendo vya ukatili. Hayo yameelezwa leo mjini Kilwa Kivinje na mratibu wa mradi wa okoa maisha ya mtoto mchanga kutokana na sababu zonazoepukika, Pius Phinias wakati wa mafunzo kwa wanajamii wa kata za Mingumbi, Kivinje na Pande.

Mafunzo ambayo yameandaliwa na kituo cha msaada wa kisheria mkoa wa Lindi (LIWOPAC) kwa ufadhili wa mfuko wa asasi za kiraia (Foundation for Civil Society). Phinias alisema kituo hicho kimekuwa kikipokea kesi nyingi za ukatili na unyanyasaji wa kijinsia zinazo angukia kwenye makosa ya jinai kutoka kwa wanawake, ambayo kituo hicho hakina uwezo wala mamlaka ya kushugulikia. Badala yake kimekuwa kinatoa msaada wa kuwashauri waende kwenye vyombo vya sheria wakafungue mashitaka.

Hata hivyo wanawake hao wamekuwa wakikataa kwa hofu kwamba wanaume zao wataadhibiwa na kupata lawama kutoka kwa ndugu za wanaume hao. Mratibu huyo alisema hali hiyo inasababisha kazi ya kukomesha ukatili wa kijinsia kuwa ngumu mkoani humu.

“Unaweza kumkuta mwanamke amefanyiwa ukatili anakimbilia kwa wasaidizi wetu wa msaada wa kisheria, wakishauriwa waende wakaripoti polisi au mahakamani wanakataa. Wanasema wanaume zao wakifungwa watapata lawama kutoka kwa ndugu na majirani,” alisema Phinias.

Aidha mratibu huyo alitoa wito kwa serikali kuangalia upya sheria ya mirathi ili ifanyiwe marekebisho. Kwasababu sheria iliyopo inaleta mgongano kutokana na watumiaji kuchanganya matumizi baina ya sheria za kimila, kidini na serikali.

“Watu wa dini mbili tofauti anapofariki mmoja wapo kunakuwa na kazi ngumu katika kugawa mirathi. Sheria za kimila hazimpi mtoto wa kike haki ya kurithi na nyingine zinampa kiasi kidogo kiliko mtoto wa kiume,” aliongeza kusema Phinias.

Kutokana na hali hiyo alitoa wito wa kuangalia uwezekano wa kutengenezwa sheria moja ya jumla itakayo tumiwa na watu wa imani zote. Kuhusu mradi wa okoa maisha ya mtoto mchanga mwenye umri wa siku 0 hadi 7, mratibu huyo alisema kituo hicho kinashugulikia masuala ya haki za watoto na wanawake. Hivyo watoto walio tumboni na wachanga wanasitahili kutetewa. Ikiwamo kuwakoa katika vifo vinavyo epukika.

Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo ya siku mbili waliiomba serikali kutengeneza sheria itayowabana wanaume wanaowapa mimba wanawake na kuzikataa. Mtendaji kata wa kata ya Mingumbi, Haji Limba alisema ilikupunguza watoto wa mitaani na magonjwa yanayoepukika ni muhimu wanaume wabanwe kwa mujibu wa sheria wakubali mimba wanawapa wanawake na wakubali kwenda kupimwa maambukizi na wanawake wanaowapa mimba.

Nae Tatu Kamtande wa Kivinje alitoa wito kwa serikali kuvisaidia vitendea kazi vikosi kazi na kamati mbalimbali za hiari ambazo zinajitolea kutoa elimu kwa jamii kuhusu usafi na afya. Kwasababu miongoni mwa sababu zinazochangia vifo vya watoto wachanga na akinamama wajawazito ni magonjwa yanayoepukika na kusababishwa na uchafu. Ikiwamo malaria.

“Mwitikio wa wawanachi ni mkubwa sana, lakini changamoto ni vitendea kazi, hata vifaa vya kuhifadhia taka mitaani havipo,” alisema Kamtande. Washiriki wengine pia waliiomba serikali kuyasaidia mashirika yasio ya kiserikali kufikisha elimu vijijini, ambako pia kuna migogoro mingi ya ardhi, ndoa na mirathi.

_______________________________________

JOIN US IN ALL SOCIAL NETWORK

Dont Miss anything!! Follow us at FacebookTwitter and Instagram for more all Infortainment !! Dont Miss to Join us at Youtube Download our Application PLAYSTORE

Tupia Comment Yako, Matusi Hapana

Recommended for you