AFYA

WANAWAKE KILWA WASHAURIWA WAJIAMINI NA KUDAI HAKI ZAO ZA MSINGI

on

Na. Ahmad Mmow, Kilwa Masoko.

Wanawake wilayani Kilwa mkoa wa Lindi, wameaswa wajiamini na kudai haki zao za msingi wanapohisi hawapewi. Wito huo umetolewa leo mjini Kilwa Masoko na mkuu wa wilaya hiyo, Christopher Ngubiagai kwenye hafla ya uzinduzi wa jukwaa la wanawake wa wilaya ya Kilwa, linalotambulika kwa jina la Tumaini Jipya la Wanawake wa Kilwa (TUJIWAKI).

Ngubiagai ambae kabla ya kutoa wito huo alilishukuru shirika la kimataifa la misaada la Action Aid kwa juhudi kubwa za kuunga mkono juhudi za serikali katika mipango ya maendeleo katika sekta mbalimbali za umma wilayani humo, alisema wanawake wanatakiwa kujiamini ili waweze kufikia malengo ya maendeleo wanayojiwekea. Alisema licha ya kujiamini lakini pia wanatakiwa kuhoji na kudai haki zao za msingi pindi wanapohisi kunadalili za kupindishwa au kutopewa.

Alisema wanawake sio dhaifu kama baadhi ya watu wanaoamini mfumo dume wanavyojaribu kuwapotosha wapenda usawa. Hivyo wanatakiwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa huku wakiamini hakuna kinachoweza kushindwa kufanyika kwasababu ya jinsia yao.

“Msijione wanyonge na kulalamika, fanyeni kazi kwa ajili ya maendeleo yenu na taifa. Kuwa mwanaume sio kigezo cha kwamba unaweza kila kitu, yapo mambo makubwa yanafanywa kwa ufanisi na wanawake, wakati wanaume hawawezi,” alisema Ngubiagai.

Aliongeza kusema dhana ya kuwaona wanawake kama raia wa daraja la pili katika nchi yao haina budi kupigwa vita na kila mpenda usawa. Kwasababu dhana hiyo inapalilia dhuluma kwa wanawake. Aidha mkuu huyo wa wilaya aliwaasa wanawake hao kurejesha mikopo kwa wakati ili wengine wasiopata waweze kukopeshwa.

Nae mratibu Action Aid wilayani humo, Steven Benard, alisema shirika hilo linatambua umuhimu wa kuchangia shuguli za maendeleo. Kwani miongoni mwa wajibu wake ni kuisadia jamii iweze kufikia malengo ya maendeleo yake na nchi. Huku akihaidi kuwa bega kwa bega na serikali kuhakikisha wanawake wanapata haki zao za msingi, kupambana na unyanyasaji wa kijinsia na ukatili dhidi yao.

Kwa upande wake katibu wa jukwaa hilo, Pili Kuliwa alisema uanzishwaji wa jukwaa hilo umetokana na kuguswa na changamoto mbalimbali zinawakabili wanawake wakiwa hawana chombo kimoja kinachowaunganisha na kutumia kupaza sauti zao. Aliyataja baadhi ya madhila wanayokumbana nayo kuwa ni ukatili wa kingono, usambazaji picha chafu mitandaoni, ndoa za utotoni na ukatili wa kiuchumi. Ikiwamo kutoshirikishwa katika kupanga matumizi ya mali ambazo zinazalishwa kwa pamoja na wanandoa na dhuluma katika mgawanyo wa mirathi.

Pia katibu huyo alitoa wito kwa mamlaka zinazohusika zitoe mikopo inayokidhi mahitaji ili waweze kumudu kufikia malengo. Kwasababu kiasi cha mikopo kinachotolewa hakitoshi kutekeleza miradi wanayopanga.

“Action Aid wamejitahidi sana wametoa mchango mkubwa katika uwezeshaji wa uanzishwaji wa jukwaa hili, lakini pia wamesaidia vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na vifaa vya ofisi. Ndio waliotoa mafunzo kwetu,” alisema Kuliwa.

Action Aid katika wilaya hiyo limekuwa na mchango mkubwa katika sekta mbalimbali, ikiwamo sekta ya elimu.

___________________________________

JOIN US IN ALL SOCIAL NETWORK

Dont Miss anything!! Follow us at FacebookTwitter and Instagram for more all Infortainment !! Dont Miss to Join us at Youtube Download our Application PLAYSTORE

Tupia Comment Yako, Matusi Hapana

Recommended for you