Kitaifa

Waendesha Pikipiki na Bajaji Lindi Wagoma Kutoa Huduma.

on

 Na. Ahmad Mmow. Lindi

Waendesha pikipiki na Bajaji katika manispaa ya Lindi, leo wamegoma kutoa huduma ya kusafirisha abiria kutokana na kile kinachodaiwa kuchoka kuonewa na askari wa usalama barabarani. Akizungumza na Lindiyetu.co.tz mwenyekiti wa waendesha pikipiki na bajaji wa kituo kikuu cha mabasi, Mjinja Sabi, alisema wamelazimika kufanya mgomo huo ili kuzijulisha mamlaka za juu za utawala baada ya juhudi zao za kutafuta ufumbuzi wa madhila wanayopata kutoka kwa asikari wa usalama barabarani kushindikana.

Huku akibainisha kwamba viongozi wa waendesha Bajaji wamefanya juhudi za kurekebisha hali ya mambo imeshindikana. Ikiwamo kwenda kwa mkuu wa wilaya ya Lindi mara kadhaa. Alisema askari hawafanyi kazi zao katika mazingira ya urafiki. Bali imekuwa kama maadui nakusababisha wafanye kazi kwa hofu. Alitolea mfano kutozwa faini mara kwa mara kwa ajili ya stika.

“Stika kwa mara ya mwisho zilitolewa mwaka jana mwezi Oktoba, siku ya wiki ya nenda kwa usalama, wengine wamenunia pikikipiki na Bajaji baada ya mwezi huo. Wakiwapa shilingi 1000 ili wapewe stika wanakataa nakuwaandikia faini ya shilingi 30000.00. Nibiashara inayoendelea na hajulikani mwisho wake utakuwa lini,” alisema Sabi.

Moja ya Kituo cha Bodaboda Mkoani Lindi eneo la Uwanja wa Fisi likiwa Tupu kabisa.

Aliongeza kusema hata wanapokuwa barabarani badala ya kuanza kuambiwa makosa wanapigwa. Sabi alikiri kuwa wapo waendesha vyombo hivyo ambao ni wakorofi. Lakini ukorofi wawachache usiwe sababu ya kuonewa wote.

“Matatizo ni mengi, ndio sababu tumeamua kugoma ilikufikisha ujumbe kwa mamlaka za juu zisikie kilio chetu, wananchi watusamehe tunajua wanapata shida kwasababu ya mgomo huu. Lakini hakuna njia nyingine ingawa tunawahurumia,” aliongeza kusema Sabi.

Baadhi ya wananchi walikiri kuwa mgomo huo umeanza kuwaathiri. Mwanaharusi Abdurhaman wa mtaa wa Mikumbi alisema alilazimika kukodi taksi kwenda hosipitali ya mkoa. Huku akibainisha kwamba watu wengi wanatembea kwa miguu. Bwana Issa Makota wa kijiji cha Nanganga alisema alilazimika kutoka kituo cha mabasi kwenda na kurudi hospitali ya Sokoine kwa miguu. Yusuf Amouri aliyetokea Dar-es-Salaam alisema analazimika kwenda kwa miguu mtaa wa Mlandege wanakoishi wenyeji wake.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Lindi, Renatha Mzinga alikiri kusikia mgomo na malalamiko hayo. Alihaidi kuyafanyia kazi. Kwa upande wa mkuu wa wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga hakuweza kupatikana hewani hadi habari hii inaandikwa.

_______________________________________________________________________

IPAKUE APPLICATION YA LINDIYETU.CO.TZ ILI USIPITWE NA STORY KALI KILA SIKU

Tupia Comment Yako, Matusi Hapana

Recommended for you

Leave a Reply