Kitaifa

Waziri Kalemani ataka umeme wa dharura Mtwara

on

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhakikisha linashughulikia haraka tatizo la kukatika kwa umeme katika mkoa wa Mtwara ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao za kiuchumi kama kawaida.Waziri Kalemani alitoa agizo hilo jana (tarehe 12 Oktoba, 2017) alipofanya kikao na Watendaji wa Wizara ya Nishati, Wenyeviti wa Bodi na Watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Kampuni ya Undelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC).

Wengine waliohudhuria kikao hicho walikuwa ni pamoja na Naibu Waziri, Subira Mgalo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo, Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga, wakandarasi wa miradi ya usambazaji wa umeme vijijini inayosimamiwa na TANESCO na REA pamoja na wasambazaji wa nyaya, nguzo na transfoma nchini.

Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kujitambulisha, kujadili namna ya kutekeleza miradi ya umeme nchini pamoja na changamoto zake. Alisema kumekuwepo na tatizo la kutopatikana kwa umeme wa uhakika katika mkoa wa Mtwara ambapo ndio chanzo cha gesi asilia inayotumika kuzalisha umeme.

Alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Dkt. Tito Mwinuka kuhakikisha unapatikana umeme wa dharura kwa namna yoyote na kuongezwa katika mkoa wa Mtwara hivyo kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme kwa mara kwa mara.

Alisema mbali na kuweka umeme wa dharura, shirika hilo linatakiwa kuhakikisha mitambo iliyoharibika inakarabatiwa mapema ipasavyo na kuendelea na mchakato wa ununuzi wa mitambo mipya kwa kasi kubwa ili hatimaye tatizo la umeme katika mkoa wa Mtwara liwe historia.

“Wananchi wa Mtwara wanateseka sana kutokana na tatizo la kukatika kwa umeme la mara kwa mara linaloukabili mkoa wao, ni jukumu la TANESCO kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika, na utekelezaji uanze mara moja,” alisema Dkt. Kalemani.

Katika hatua nyingine, Waziri Kalemani alisema kuwa Shirika la Tanesco linatarajiwa kuanzisha vituo vidogo vidogo kwenye kata na tarafa ambavyo vitakuwa kwa ajili ya kuunganishia wakazi umeme.
Alisema vituo hivyo vitakuwa rasmi kwa ajili ya wateja kuhudumiwa kwa kukutana na watumishi wa Tanesco moja kwa moja badala ya kukutana na vishoka wanaojifanya ni watumishi wa Tanesco ambao huwatoza gharama kubwa na kuwalaghai.

Aidha aliwataka wananchi kufuata taratibu za kuunganishiwa umeme kwa kuwa wameondoa ada ya maombi hivyo wasiogope kuleta maombi wakidhani kuwa watatozwa bili yoyote.
Akielezea mikakati yake tangu kuteuliwa kuwa Waziri wa Wizara Mpya ya Nishati, Dkt. Kalemani alisema ameweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa umeme wa uhakika unapatikana kwa gharama nafuu nchi nzima.

Alitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa umeme unaozalishwa unafikia Megawati 5000 ifikapo mwaka 2020 ikiwemo ujenzi wa njia za kusafirisha umeme za kilovolti 400 kwenye kanda zote nchini.
Wakati huohuo, Waziri Kalemani aliwataka wakandarasi waliokabidhiwa miradi ya REA Awamu ya Tatu kuanza kazi mara moja na kuhakikisha kuwa miradi inakamilika kwa wakati.

Naye Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalo alitoa pongezi wa serikali kujali watoa huduma wa ndani wa usambazaji wa vifaa vya umeme kama vile nguzo, nyaya na transfoma na kuwaomba kujikita kwenye uzalishaji wa bidhaa hizo hapa nchini na kuimarisha sekta ya viwanda nchini.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inaunga mkono uwekezaji wa viwanda ili kuhakikisha kuwa sekta ya viwanda inakuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi na kuwa miongoni mwa nchi zenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.


IPAKUE APPLICATION YA LINDIYETU.CO.TZ ILI USIPITWE NA STORY KALI KILA SIKU

Tupia Comment Yako, Matusi Hapana

Recommended for you

Leave a Reply