News

Watumishi Watakiwa Kuboresha Mifumo ya Ukusanyaji Mapato ya Serikali

Na Farida Ramadhani & Josephine Majura. WFM, Dodoma

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, Watumishi wa wizara hiyo kuendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji mapato ya ndani na kupanua wigo wa walipakodi pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato kutoka vyanzo mbalimbali.

Watumishi Watakiwa Kuboresha Mifumo ya Ukusanyaji Mapato ya Serikali

Dkt. Kijaji ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Kambarage, wizarani hapo.

Alisema Wizara ya Fedha na Mipango imebeba majukumu ya  kuhakikisha kuwa mapato ya Serikali na matumizi ya rasilimali fedha yanasimamiwa kikamilifu.

 “Watendaji na watumishi wote wa Wizara wanawajibu wa kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha na ufuatiliaji wa matumizi ili kuhakikisha rasilimali fedha zilizopo zinatumika kwa ufanisi” ,alisema Dkt. Kijaji.

Alisema ni jukumu la Watumishi wa Wizara kugawa rasilimali fedha kwa kuzingatia vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016-2021)  wenye dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu.

Watumishi Watakiwa Kuboresha Mifumo ya Ukusanyaji Mapato ya Serikali

Aliwataka Watumishi  kufanyakazi kwa ushirikiano, umoja, mshikamano, ufanisi  na uadilifu kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali iliyopo.

“Ni wajibu wetu pia kutumia busara na hekima, hususan pale tunaposhughulikia maslahi ya watumishi na wananchi kwa ujumla”, alisisitiza Dkt. Kijaji.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ambaye pia ni  Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, Bw. Doto James, amemhakikishia Dkt. Kijaji kuwa watatekeleza maelekezo yote aliyoyatoa kwa haraka na ukamilifu kwa maendeleo ya nchi kwa kuwa Wizara hiyo ni nguzo ya kusimamia uchumi wa nchi.

Alisema uzoefu unaonesha kwamba vikao vya Baraza la wafanyakazi vimekua na umuhimu mkubwa mahala pa kazi na kwa kuzingatia umuhimu huo Wizara ya Fedha na Mipango imehakikisha kuwa vikao vya Baraza vinafanyika kila mwaka kulingana na Mkataba kati ya Wizara na Chama cha Wafanyakazi cha Serikali na Afya (TUGHE).

Alisema kupitia Baraza la wafanyakazi Wizara imefanikiwa kuongeza mshikamano kati ya Wafanyakazi hivyo kuamsha ari kwa watumishi kufanya kazi kwa kushirikiana na Viongozi wa Serikali.

Aliongeza kuwa hoja mbalimbali zilizowasilishwa kwenye Baraza zimeboresha huduma kwa watumishi, kuboresha mazingira ya kufanyia kazi ikiwemo kuwapatia watumishi vitendea kazi pamoja na kuwelimisha watumishi kuhusu magonjwa sugu kama vile kisukari, shinikizo la damu (BP), Kifua kikuu, HIV na UKIMWI.

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAPANA)
Tags
Show More

Related Articles

Close

Adblock Detected

Please consider supporting us by disabling your ad blocker